Kwa kiasi fulani ningeliweza kutafuta njia ya kupandikiza
ndani ya akili ya mtoto shauku yangu kuu ya kupata njia na namna ya kufikisha
sauti kwenye ubongo wake bila ya kutumia masikio.
Pindi tu mtoto angefikisha umri wa kutambua, ningeliweza
kuijaza akili yake kikamilifu kwa shauku kuu ya kusikia kiasi kwamba asili
kwa kutumia njia zake yenyewe ingeweza kuitafsiri kuwa ukweli wenye kuonekana.
Fikra zote hizi zilitokea ndani ya akili yangu mwenyewe, na sikumwambia mtu
yeyote. Kila siku nilirudia tena upya ahadi niliyokuwa nimejiwekea mwenyewe ya
kutokukubali ububu-kiziwi kwa kijana wangu.
Kwa kadiri alivyokuwa akikua na kuanza kutambua mazingira
yaliyomzunguka , tuligundua kuwa alikuwa na uwezo kidogo wa kusikia.
Alipofikisha umri ambao kwa kawaida watoto huanza kuzungumza, hakuonesha dalili
za kuzungumza, lakini tuliweza kutambua kupitia vitendo vyake kwamba aliweza
kusikia baadhi ya sauti kidogo. Hicho ndicho nilichokuwa nataka kufahamu! Nilishawishika kwamba, ikiwa
aliweza kusika, hata kama ni kwa kiasi kidogo angeliweza bado kuongeza uwezo
mkubwa zaidi wa kusikia.
Halafu, kitu fulani kilitokea ambacho kilinipa matumaini.
Kilitoka kwa chanzo ambacho hakikutegemewa kabisa- tulinunua record
player, mtoto aliposikia muziki kwa mara ya kwanza, alijawa na furaha
ya ajabu, na mara moja aliikubali ile mashine. Haraka alionyesha mapenzi kwa
baadhi ya rekodi, miongoni mwao ni, ‘It’s a long way to Tipperary’.
Katika tukio moja, alikicheza kibao hicho tena na tena kwa karibu saa mbili,
akiwa amesimama mbele ya record player
huku meno yake akiwa ameyakita ukingoni mwa kasha la player.
Umuhimu wa tabia hii aliyojijengea mwenyewe
haukujidhihirisha wazi kwetu mpaka miaka ya baadaye kwani kwa wakati ule
hatukuwa tumewahi kusikia kanuni ya “Sauti kusafiri kupitia mfupa(bone conductivity of sound).
Muda mfupi baada ya kuwa ameikubali ile record player,
niligundua kwamba aliweza kunisikia vyema nilipozungumza midomo yangu ikiwa
imegusa mfupa wake nyuma ya sikio, au kichwani chini ya ubongo.
Ugunduzi huu ulinifanya niwe na nyenzo muhimu ambazo kwa
kupitia hizo nilianza kutafsiri kuwa kweli Shauku yangu kuu ya kumsaidia kijana
wangu kutengeneza uwezo wa kusikia na kusema.
Kipindi hicho alikuwa akijaribu kwa shida kusema baadhi
ya maneno. Mwelekeo haukuwa unaridhisha lakini shauku ikisaidiwa na imani
haijui neno liitwalo “haiwezekani”
Baada ya kujiridhisha kwamba alikuwa anaweza kusikia
sauti yangu vizuri, nilianza mara moja kuhamishia kwenye akili yake shauku ya
kusikia na kusema. Haraka niligundua kwamba mtoto alikuwa akifurahia hadithi
wakati wa usiku, hivyo nilianza kazi ya kutunga hadithi zenye kumjengea hali ya
kujitegemea, ubunifu na hamu kubwa ya kusikia na kuwa katika hali ya kawaida.
Kulikuwa na hadithi moja mahsusi ambayo niliiwekea
msisitizo kwa kuipamba kwa nakshi mpya kila wakati iliposimuliwa. Ilitengenezwa
kupandikiza kwenye akili yake mawazo kwamba hali yake ya ulemavu haikuwa ni
mkosi bali ilikuwa ni rasilimali yenye thamani kubwa.
Licha ya ukweli kwamba falsafa zote nilizokuwa nimezichunguza
vyema zilionyesha kwamba kila mkosi huja ukiwa ndani yake umebeba mbegu ya neema inayolingana na mkosi
wenyewe, ni lazima nikiri kwamba
sikuwa na wazo hata kidogo la jinsi ambavyo huu ulemavu ungeweza
kubadilika kuwa rasilimali.
Hata hivyo niliendelea na kitendo cha kuifungasha hiyo falsafa ndani ya hadithi za usiku
nikitumaini kuwa muda ungeweza kufika
ambapo angeweza kupata njia ambayo ulemavu wake ungeliweza kubadilishwa ukaweza
kutumika kwa malengo yenye manufaa.
Mantiki iliniambia wazi kuwa kulikuwa hakuna mbadala wa
kutosha wa upungufu wa uwezo wa asili wa kusikia. Lakini Shauku ikisaidiwa na Imani iliisukuma
mantiki pembeni, na kunitia moyo kuendelea mbele.
Nikichanganua uzoefu huo kwa kufikiria ya nyuma, naweza
kuona sasa kwamba imani ya kijana wangu kwangu ilikuwa na dhima kubwa kwa
matokeo hayo ya kushangaza. Hakuhoji chochote kile nilichomwambia. Nilimuuzia
wazo kwamba alikuwa na fursa ya kipekee kumshinda kaka yake, na hivyo fursa
hiyo ingeweza kujiakisi yenyewe kwa namna nyingi.
Kwa mfano waalimu shuleni wangeweza kuona kuwa alikuwa
hana masikio, na kwa sababu hiyo, wangeliweza kumpa uangalizi wa kipekee na
kumtendea wema usiokuwa wa kawaida. Walifanya hivyo mara zote. Mama yake
alilihakikisha hilo kwa kuwatembelea walimu na kupanga nao kumpa mtoto
uangalizi wa ziada uliohitajika.
Nilimuuzia wazo pia kwamba wakati atakapokuwa na umri wa
kutosha kuuza magazeti (kaka yake alikuwa tayari ameshaanza kuuza magazeti)
angeweza kuwa na fursa ya kipekee kumshinda kaka yake kwani watu wangeliweza
kumlipa pesa za ziada kwa huduma zake kwa sababu wangeweza kuona
alikuwa ni mwenye akili, kijana mchapakazi, licha ya sababu kwamba alikuwa hana
masikio.
Tuligundua kwamba, taratibu uwezo wa mtoto kusikia
ulikuwa ukiongezeka. Zaidi ya hapo, hakuwa na kawaida yeyote ya kujitambua
binafsi juu ya ulemavu wake. Alipofikisha miaka saba alionyesha ushahidi wa
kwanza kuwa njia yetu ya kuboresha akili yake ilikuwa inazaa matunda.
Kwa kipindi cha miezi kadhaa alikuwa akiomba apewe ruksa
ya kuuza magazeti, lakini mama yake asingeweza kumpa ruksa, alikuwa anaogopa
kwamba uziwi wake ungesababisha hatari kwa yeye kuingia barabarani mwenyewe.
Mwishowe jambo hili aliamua alifanye peke yake. Mchana mmoja alipoachwa
nyumbani na mfanyakazi, alipanda kupitia dirisha la jiko, akarukia chini na
kuanza kivyake.
Alikopa senti sita za mtaji kutoka kwa jirani yao
aliyekuwa fundi viatu, alipata faida senti 42. Tulipofika nyumbani usiku ule,
tulimkuta kitandani akiwa amelala huku mkononi akiwa ameshikilia kwa nguvu zile
pesa. Mama yake aliufungua ule mkono wake, akaondoa sarafu na kisha kulia.
Katika yote, kulia juu ya ushindi wa kwanza wa mwanawe,
ilionekana siyo sahihi. Mrejesho wangu ulikuwa kinyume. Nilicheka sana, kwani
nilijua kwamba juhudi zangu kupandikiza ndani ya akili ya mtoto mtazamo wa
kujiamini zilikuwa zimefanikiwa. Mama yake alichokiona katika ujasiriamali wake
huu wa mwanzo ni; mvulana mdogo kiziwi ambaye alikuwa ameingia barabarani na
kuhatarisha maisha yake ili kupata pesa.
Nilichokiona ni; mfanyabiashara mdogo jasiri, mwenye nia,
mwenye kujitegemea ambaye uwezo ndani yake ulikuwa umeongezeka kwa asilimia 100
kwa kuwa alikuwa ameingia kwenye biashara akitumia uwezo wake mwenyewe, na
alikuwa amefanikiwa. Mwamala uliniridhisha kwa sababu nilijua alikuwa ametoa
ushahidi wa sifa ya uwerevu ambayo ingeweza kumkaa maisha yake yote. Matukio ya
baadaye yalikuja kuthibitisha hili kuwa kweli.
Kaka yake alipotaka kitu fulani angeweza kugharaghara
chini, kurusharusha miguu yake hewani akilia
mpaka akipate. Wakati “mvulana mdogo kiziwi” alipotaka kitu, angeweza
kupanga jinsi ya kupata pesa, na kisha kujinunulia mwenyewe. Bado anaendelea
kufuata njia hiyo!
Ukweli, kijana wangu mwenyewe amenifunza ya kuwa ulemavu
unaweza ukageuzwa kuwa mawe ya kuvukia , ambayo mtu anaweza akayatumia kupanda
kufikia malengo yenye thamani ikiwa hautapokewa kama kikwazo na kutumiwa kama
kisingizio.
Mvulana mdogo kiziwi alipita madarasa, sekondari na chuo
pasipo kuweza kuwasikia walimu wake, isipokuwa pale walipopaza sauti kwa nguvu,
wakiwa karibu. Hakwenda shule ya viziwi. Tusingeliweza kumruhusu kujifunza
lugha ya ishara. Tulidhania kwamba, alipaswa kuishi maisha ya kawaida na
kushirikiana na watoto wa kawaida, na tuliusimamia uamuzi huo, ingawa
ulitugharimu mijadala mingi mikali na maafisa wa shule.
Kipindi alipokuwa sekondari, alijaribu vifaa vya kusikia
vya umeme, lakini havikuwa na manufaa yeyote kwake. Tuliamini hii ilitokana na
hali iliyogundulika wakati mtoto alipokuwa na umri wa miaka sita. Daktari J.
Gordon Wilson wa Chicago alimfanyia mtoto upasuaji katika upande mmoja wa
kichwa chake na kugundua kwamba hakukuwa na dalili ya viungo vya asili vya
kusikia.
Katika juma lake la mwisho chuoni (miaka 18 baada ya
upasuaji) kitu fulani kilitokea ambacho kiliweka alama katika hatua muhimu
zaidi ya maisha yake. Kupitia kile kilichoonekana kutokea kwa bahati, alikuja
kuwa na kifaa kingine cha umeme cha kusikia ambacho alitumiwa kwa ajili ya
majaribio.
Alikuwa mzito katika kukijaribu kutokana na kuvunjwa moyo
na kifaa kingine kama hicho. Mwishowe aliinua kile kifaa kama vile hataki na
kukiweka kichwani, akafunga betri, na lo!
kama vile kwa pigo la mazingaombe, HAMU YAKE YA MUDA MREFU YA KUSIKIA
KAWAIDA ILIKUWA IMEGEUKA KUWA KWELI! Kwa
mara ya kwanza katika maisha yake alisikia kama mtu mwingine yeyote yule mwenye usikivu wa kawaida.
“Mungu hutenda kwa namna ya ajabu”. Akiwa na furaha
iliyopindukia kutokana na Ulimwengu tofauti ulioletwa kwake kupitia kifaa chake
cha kusikia, alikimbia kwenye simu akampigia mama yake, na kusikia sauti yake
vizuri. Siku iliyofuata aliisikia barabara sauti ya profesa wake darasani kwa
mara ya kwanza katika maisha yake! Alisikiliza redio. Alisikiliza sinema. Kwa
mara ya kwanza katika maisha yake, aliweza kuwasiliana kwa uhuru na watu
wengine pasipo wao kupaza sauti.
.....................................................................................................
0 Response to "MUNGU HUTENDA KWA NAMNA YA AJABU !"
Post a Comment