WAOTA NDOTO KIVITENDO HUWA HAWAKATI TAMAA | JIFUNZE UJASIRIAMALI

WAOTA NDOTO KIVITENDO HUWA HAWAKATI TAMAA

...............inatoka sehemu ya iii
Ikiwa kitu unachotaka kufanya ni sahihi, na unakiamini, endelea kufanya! Iweke ndoto yako mbele, na kamwe usijali kile “wanachokisema” ikiwa utakutana na anguko la muda, kwa kuwa labda, hawafahamu kwamba, kila anguko huja likiwa limebeba mbegu ya mafanikio yenye ukubwa sawa na anguko lenyewe.
  
Henry Ford, aliyekuwa masikini na ambaye hakuwa na elimu, aliota juu ya gari lisilokokotwa kwa farasi. Alikwenda kufanya kazi akitumia zana alizokuwa nazo pasipo kusubiri fursa nzuri imjie, na sasa ushahidi wa ndoto yake umetapakaa duniani kote. Ameyafanya matairi mengi zaidi kuzunguka kushinda mtu mwingine yeyote yule aliyewahi kuishi kwasababu hakuwa mwoga kuzisukuma mbele ndoto zake.

Thomas Edison aliota ndoto ya taa ambayo ingeweza kuwaka kwa kutumia umeme. Licha ya kufeli mara elfu kumi, aliisimamia ndoto yake hiyo mpaka ilipogeuka kuwa kitu halisi. Waotaji ndoto kivitendo huwa hawakati tamaa!  

Lincoln aliota ndoto ya Uhuru kwa watumwa weusi, akaiweka ndoto yake katika vitendo, na kwa bahati mbaya alifariki kabla ya kuiona Kaskazini  na Kusini zikiungana zikiitafsiri ndoto yake kuwa kweli.
Wright Brothers(waliokuwa ndugu wawili) waliota ndoto ya mashine yenye uwezo wa kuruka kupitia angani. Sasa mtu anaweza  kuona ushahidi duniani kote kwamba walichokiota kilikuwa sahihi. Marcon aliota ndoto ya mfumo kwa ajili ya kuzitumia nguvu zisizoshikika zilizopo juu angani. Ushahidi kwamba hakuota ndoto bure, unaweza ukaonekana katika kila redio, TV na simu za mkononi duniani.

Si hivyo tu ndoto ya Marcon ilizileta nyumba za hali ya chini kabisa  kuwa kandokando ya majumba makubwa ya kifahari. Ilifanya watu wa kila Taifa juu ya Dunia kuwa jirani kwa kutengeneza njia ya mawasiliano ambapo habari, taarifa na burudani ziweze kusambazwa mara moja dunia nzima

Inaweza kukuvutia kujua kwamba “marafiki” wa Marcon walimchukua na kumweka kizuizini, na kumchunguza katika hospitali ya magonjwa ya akili wakati Marcon alipotangaza kwamba alikuwa amegundua kanuni ambayo angeweza kuitumia kutuma ujumbe kupitia hewani pasipo kutumia waya wala njia nyingineyo inayoweza kushikika ya mawasiliano.

Waotaji ndoto wa leo wanatendewa vyema. Dunia si ngeni tena kwa ugunduzi mpya. Kwa kweli imeonyesha utayari wa kuwalipa waotajindoto ambao huipa Dunia wazo jipya. Dunia imejazwa fursa tele ambazo waotajindoto wa zamani kamwe hawakuzijua. Shauku kubwa ya kuwa na kutenda ni alama ya kuanzia ambayo muotajindoto ni lazima aanzie.

Ndoto hazizaliwi hivihivi tu kivivu pasipokuwa na malengo. Dunia haiwakejeli tena waotajindoto, wala kuwaita ni wenye maneno matupu yasiyotekelezeka. Kumbuka pia kwamba wale wote wanaofanikiwa katika maisha, huanzia na mwanzo mbaya, na kupitia mapambano mengi yenye kuumiza moyo kabla “hawajafika”.

 Kipindi muhimu katika maisha ya wale wanaofanikiwa kwa kawaida huja katika kipindi cha matatizo, ambapo kupitia kwayo hujitatambulisha “nafsi zao za pili”. John Bunyan aliandika “The Pilgrim’s Progress”(Maendeleo ya Mahujaji) baada ya kuwa amefungiwa gerezani na kupewa adhabu kali kutokana na mtazamo wake wa kidini.

O. Henry alikigundua kipaji kilichokuwa kimelala ndani ya ubongo wake baada ya kukutana na mkosi mkubwa, na alifungiwa ndani ya chumba cha gereza huko Columbus, Ohio. Kwa kusukumwa na hali ngumu aliyokuwa akiipitia kutambua “nafsi yake ya pili” na kwa kutumia ubunifu wake, aligundua mwenyewe kwamba alikuwa mwandishi mkubwa badala ya mhalifu mwenye mateso na aliyetengwa na jamii.


Njia za maisha zipo za aina nyingi na za ajabu na bado uwezo usiokuwa na kikomo ni wa ajabu ambapo kupitia huo watu wakati mwingine hulazimika kupitia kila aina ya adhabu kabla ya kugundua akili zao na uwezo wao wenyewe wa kuzalisha mawazo yenye manufaa kupitia ubunifu.

Itaendelea sehemu ya tano (v)..............................







0 Response to "WAOTA NDOTO KIVITENDO HUWA HAWAKATI TAMAA"

Post a Comment