KWANINI MPANGO WA BIASHARA WA KUANDIKIWA SIYO MZURI KWAKO? | JIFUNZE UJASIRIAMALI

KWANINI MPANGO WA BIASHARA WA KUANDIKIWA SIYO MZURI KWAKO?

Mpango mzuri wa biashara ni ule unaouandika mwenyewe na wala siyo wa kuandikiwa na mtaalamu au mtu mwingine yeyote yule. Hata ikiwa utaandikiwa na mtaalamu lakini unashauriwa kuhakikisha kwamba angalao vitu vyote vya msingi unaviandaa mwenyewe, siyo lazima katika mpangilio maalumu, lakini uwe na picha ya kile unachotaka kiandikwe kwa mfano mauzo yako unakadiria yatakuwa kiasi gani, mtaji, nk.

Mpango wa biashara ni kama jino au kiungo fulani cha mwili wako, ikiwa linauma huwezi ukamwambia mwenzako akangoe la kwake na kisha ndipo la kwako lipone, hapana, jino ni la kwako kwa hiyo anayeyajua maumivu yake ni wewe, na ni lazima wewe mwenyewe ndiye utakayehusika katika kulipatia matibabu.

Anayeijua biashara yako zaidi ni wewe mwenyewe na wala siyo mtaalamu au mshauri wa biashara, malengo, mikakati, mauzo, soko, na hata kiasi cha mauzo unachokisia ni wewe mwenye biashara unayevijua vizuri  zaidi kushinda mtu mwingine yeyote. Si hivyo tu bali pia Mpango wa biashara ni kitu kitakachodumu kwa muda mrefu huku kikibadilika kulingana na biashara nayo itakavyokuwa ikibadilika.

Hivyo ikiwa umeuziwa au kuandikiwa   mpango wa biashara ambao huelewi ulivyo, labda kwa lengo la kuombea fedha benki au kushawishi wabia nk., baada tu ya muda mfupi mpango ule hautakuwa na manufaa yeyote tena kwako kwani utakuwa huwezi kuubadilisha chochote kile biashara nayo itakavyokuwa ikibadilika. Utakuwa tayari umeshapitwa na wakati.

Kwa hiyo mjasiriamali hata ikiwa hupendi kujisumbua kujifunza kuandika mpango wa biashara lakini ni vizuri zaidi ukafahamu angalao masuala yale ya msingi ili utakapokuwa ukiandikiwa mpango wa biashara yako na mtu mwingine basi uwe unatoa mapendekezo ni vipi ungependa uwe kulingana na mazingira ya biashara husika na utafiti ulioufanya, kwani ni wewe utakayeendesha biashara.

Usije ukawa ni mtu wa kusema ndiyo tu kwa kila kitu hata ikiwa anayekuandikia mambo mengine amefanya ilimradi mpango ukamilike.
Kama utakodi mtu akuandikie, basi tafuta mtu atakayekuwa kama mshauri, atakayetoa mapendekezo, mtakayeshauriana  na siyo atakayebeba jukumu zima la kuandika kama lilivyo mithili ya mjenzi wa nyumba. Hivyo umuhimu wa kufahamu jinsi mpango wa biashara unavyotakiwa kuwa ni mkubwa kwa kila mjasiriamali.

------------------------------------------------------------------------------------------


*Mpenzi msomaji, unakaribishwa kuja kujipatia vitabu vyako, vya ujasiriamali kikiwamo pia na kitabu Maarufu chenye kila kozi za ujasiriamali pamoja na jinsi unavyoweza kuandika MPANGO au MCHANGANUO wa biashara yako mwenyewe cha “Jifunzemichanganuo ya biashara na Ujasiriamali” Tupigie simu zifuatazo;  “0712 202244 / 0765 553030” au fika duka lililopo Buguruni  sokoni stendi ukivuka barabara mbele kidogo ya Akiba Commercial Bank utaona bango juu ya duka lililoandikwa wakala wa vitabu vya Self Help Books.

0 Response to "KWANINI MPANGO WA BIASHARA WA KUANDIKIWA SIYO MZURI KWAKO?"

Post a Comment