KUTAFUTA SOKO LA BIDHA ZAKO, KUNAHITAJI UBUNIFU | JIFUNZE UJASIRIAMALI

KUTAFUTA SOKO LA BIDHA ZAKO, KUNAHITAJI UBUNIFU

Halima ni msichana anayefanya kazi ya kuuza katika duka moja la jumla la kuuza maji, hivi karibuni alinifuata na kutaka nimpatie ushauri ni kwa jinsi gani anaweza kukabiliana na ugumu wa maisha hasa ukizingatia kwamba mahitaji yake ni mengi kushinda kipato anachopata kutokana na ajira yake hiyo. Nyumba aliyopanga huko Kigogo Mbuyuni zamani haikuwa na umeme lakini sasa wameweka umeme, anahitaji kuwa na vifaa vya ndani kama TV nk. Lakini  mshahara peke yake haumtoshi.

Alikuwa tayari na wazo lake mwenyewe kichwani la kuanzisha vibiashara vidogovidogo, ambavyo angevifanya muda wake wa ziada na wakati akiwa katika kazi yake. Wazo la kwanza lilikuwa ni kutengeneza vitu kama karanga za kufunga, pamoja na maandazi. Mimi nilichomwambia ni kwamba, wazo lake hilo ni zuri na  biashara zote hizo zinawezekana kabisa kufanya kwani haziwezi zikaingiliana na ile ya bosi wake. Nilimtia moyo na kumhakikishia kwamba athubutu tu kwani, hakuna jambo lolote linaloweza kutokea pasipo kwanza mhusika kuchukua hatua za kulitenda.

Nilimshauri atengeneze mpango wake wabiashara japo ni kwa kuufikiria kichwani tu na wala siyo lazima auandike kwenyekaratasi, nilimfundisha kwamba, kwakuwa tayari ameshakuwa na wazo ambalo ndiyo dhamira yake kuu, atengeneze sasa malengo, na moja nilimwambia tayari alikuwa nalo ambalo ni kupata pesa kwa ajili ya kununulia tv, lingine kupata kiasi cha pesa kila mwezi za kulipia gharama ya umeme, nikamweleza anaweza akaongeza na malengo mengine aliyokuwa nayo kichwani.

Jambo lingine muhimu sana nililomweleza ni kufikiria mpango wake wa masoko utakuwaje, nilimshauri aumize kichwa kujua ni vipi atahakikisha bidhaa zake zinawafikia wateja, watajuaje kama anauza vitu hivyo, atatumia mbinu zipi na mikakati kuwavutia wateja wake hao. Sikutaka kabisa kumuonyesha mbinu hizo moja kwa moja au kumwambia afanye kitu gani kwani nilitaka abuni kulingana na mazingira yake mwenyewe ndiyo mikakati inaweza ikafanya kazi vizuri.

MATOKEO YAKE.
Halima siku ya kwanza alianza kutengeneza karanga za kufunga, na kuanza kuziuza pale kazini baada ya siku kadhaa, aliniambia amebadilisha mkakati, na hatauzia tena pale kazini, badala yake amebuni soko jingine huko nyumbani anakoishi, ile jioni baada ya kufunga kazi, akifika nyumbani hutoka na kwenda kando kando ya barabara pana stendi ya daladala, na hapo huweka karanga zake na kuanza kuuza. Nilimshauri, badala sasa ya kuuza karanga peke yake aondeze hapo na vitu vingine kama sigara, pipi, biskuti, ubuyu, na maji ya kufunga. Ushauri wangu huo aliufanyia kazi nabaada ya siku chache akaniambia mambo yalikuwa yakienda vizuri.

AANZA KUKAANGA MAANDAZI.
Biashara imeendelea kushamiri, akaja tena na kuniambia sasa ameona aanzishe na maandazi, nilitaka nimshauri asianzishe kwanza biashara hii, kutokana na kuona kwamba kazi zingekuwa nyingi mno jambo ambalo lingeweza kumsababishia kuharibu ajira yake lakini yeye mwenyewe akadai haitaweza kuathiri kabisa majukumu yake ya kazi kwani alikuwa amedhamiria kiukweli hata ingewezekana asilale angefanya hivyo, “ usiniambie eti kazi zitakuwa nyingi huku umasikini ukiniua, mbona kabla sijaaza, nilikuwa napata muda wa kupiga stori za umbea nyumbani mpaka hata saa tano usiku, hebu niache huko” aling’aka Halima.
Akikanda unga wa maandazi
Nilimwambia basi ikiwa ataamua kuanzisha maandazi ajaribu kufikiria kwamba, biashara hii, ina ushindani mkubwa, karibu kila mwanamke wa nyumbani huifanya, sasa aumize tena kichwa na kufikiri ni kitu gani cha pekee atakachoweza kukifanya kuwashawishi wateja wawe wanakuja kununua maandazi yake na kuyaacha ya wale waliokwisha wazoea.
 Maandazi yakiwa tayari kupelekwa sokoni.
Jibu alilokuja nalo baada ya siku moja, aliniambia ya kwamba maandazi yake atakuwa akiyatia tui la nazi, ambalo huyafanya yawe na ladha nzuri na ya kupendeza mtu anapoyatafuna mdomoni. Kweli siku ya kwanza tu kutengeneza maandazi aliyapitisha pale ninapokaa na nilipoonja moja tu, nikamwambia aniongezee mengine matano, yalikuwa matamu ‘balaa!’

CHANGAMOTO.
Siku ya kwanza alitengeneza maandazi kiasi kama nusu  kilo hivi, alipoyatua chini tu na baada ya mimi kununua hapo matano, mtu wa pili alinunua maandazi 20 ya familia, mtu wa tatu hakuweza kupata idadi ya maandazi aliyokuwa akiyataka, yakawa yamemalizika.

Halima alinifuata na kuniambia huku akitabasamu, “yamekwisha na wengine wamekosa, kesho nitajaza kindoo kizima” Nilimwambia achukue tahadhari kwani biashara ya kuanza haitabiriki hata kidogo. Nilimsihi aendelee kwanza kutengeneza kiasi kile kile au hata akiongeza basi iwe ni kiasi kidogo sana mpaka atakapohakikisha ana wateja wa uhakika.

Siku iliyofuata alibeba maandazi kindoo kimejaa mpaka juu, kama kawaida walikuja wateja wale wa jana yake kakini, mpaka jua linazama bado kindoo kilikuwa kimejaa, walinunua watu wachache!  Halima akaanza kuingiwa na wasiwasi, alinifuata na aliponieleza nikamwambia awe mvumilivu kwani ndivyo biashara ilivyo, huwezi kila siku mambo yakaenda vizuri. Aliyarudisha nyumbani lakini kesho yake aliniambia kwa bahati nzuri jioni ile alikwenda kuyauza yote  pale katika kijiwe cha stendi ya daladala karibu na nyumbani kwao anakoishi.

UBUNIFU ZAIDI.
Ili kukabiliana na changamoto ya kubaki kwa maandazi mara kwa mara, Halima mwenyewe alibuni mkakati ambao hata mimi binafsi alinishangaza, mwenyewe anasema kuna siku maandazi yalibaki mengi, jioni akayatazama kwa uchungu karibu machozi yamtoke akikumbuka mtaji wake wa shida aliouwekeza pale. Akiwa anarudi nyumbani jioni hiyo, alikuwa akiwaza na kuwazua afanye kitu gani kitakachomhakikishia soko la bidhaa zake hizo. Maandazi ni mazuri, matamu na yanakidhi kila haja ya mteja lakini shida ilikuwa, ni njia ipi rahisi itakayomwezesha kuyauza?

Alipokuwa akipita maeneo ya sokoni  Ilala Boma, kichwani alikumbuka jinsi ambavyo mahali hapo muda wa asubuhi panakuwa na pilikapilika ya watu wanaofika kununua nguo kwa ajili ya kwenda kuziuza. Lilimjia wazo la kujihimu asubuhi na mapema kabla hajaja kazini, apitishe maandazi yake hapo sokoni na baada ya kuuza ikifika saa moja hivi basi aende zake kazini huku ‘mzigo’  unaokuwa umebakia aje awauzie wateja wake wa kawaida wa kila siku kazini, na hata ikiwa yatabakia tena kidogo, hayo ni lazima yakamalizike pindi atakapokuwa amefika kijiweni kwake masaa ya jioni.

Wanawake wakiuza vitafunwa sokoni (picha na Majira)
Mkakati huo Halima aliutekeleza kwa mafanikio makubwa kiasi kilichonifanya nimtanie, “Mwanamke wa shoka anatakiwa kuwa mbunifu namna hiyo na siyo kukaa tu na kusubiri” . Sasa hivi, taratibu anaanza kuzoea maisha ya kuchakarika(ujasiriamali), hasubiri tena kufanya kila kitu kwa mshahara, kazi yake inaenda vizuri, muda wa kazi hauingiliani na wa biashara zake na soko lake la maandazi halina tena vikwazo.

----------------------------------------------------------------------------------------

*Ndugu msomaji wa blogu hii, tunapenda kukutaarifu kuwa vile vitabu vilivyokuwa vimekwisha sasa vipo tayari, na vinapatikana ukiwa mahali popote pale nchini. Ikiwa utahitaji usisite kutupigia namba zetu hapo juu. Pia kama una maoni yeyote yale juu ya makala hii au chochote kuhusiana na biashara basi, yatoe hapo chini katika kisanduku cha maoni. Asante.  


0 Response to "KUTAFUTA SOKO LA BIDHA ZAKO, KUNAHITAJI UBUNIFU"

Post a Comment