HAKUNA BIASHARA ISIYOKUWA NA FAIDA | JIFUNZE UJASIRIAMALI

HAKUNA BIASHARA ISIYOKUWA NA FAIDA

Ni hivi karibuni nilikuwa nikipita katika mtaa mmoja maeneo ya Manzese Tip Top ndani ndani, nikahitaji vocha kwa ajili ya simu yangu ya mkononi, niliuliza vioski  na maduka  si chini  ya matano lakini cha ajabu kila mmoja alinijibu hauzi vocha. Nikaenda duka moja kubwa ambalo nilidhani isingekuwa rahisi kukuta hawauzi vocha  za simu. Baada tu ya kumtaka muuzaji anipe vocha ya sh. 1,000 nilishangazwa na majibu aliyonipa.

Hatuuzi vocha mjomba” muuzaduka alinijibu, na mimi ikabidi nimuulize ikiwa mtaa ule watu hawatumii simu za mkononi,  nilikuwa nimechoka baada ya kupita maduka yote  matano bila mafanikio. “Vocha labda uende kule Tip Top stendi, hazina faida kabisa mjomba, tena hasa hasa hizi za shilingi mia tano sitaki hata kuziona, shilingi 20 faida! biashara kichaa hiyo hailipi” alimaliza yule muuzaduka.

Siyo vocha za simu tu peke yake, ni biashara  za aina nyingi zinazolalamikiwa na watu kuwa hazina faida kutokana na faida yake kuwa kidogo, biashara hizo utakuta mara nyingi  ni zile ambazo asilimia ya faida ghafi katika mauzo(gross profit margin) ni kidogo, chini ya asilimia 10%.

Watu wengi hupendelea wanaponunua kitu na kukiuza hasa hasa wale wanaofanya biashara za rejareja  basi angalao pawe na asilimia 10% mpaka 25%. Hii inamaanisha kuwa, ikiwa bidhaa ameinunua kwa shilingi 2000, basi  akiiuza apate faida  angalao shilingi  200 – 400. Lakini bidhaa mfano  wa  vocha zenye faida ghafi asilimia 5%, atapata faida ghafi shilingi 100 pekee kwa vocha ya shilingi 2000.

Kitu watu wengi wasichofahamu ni kuwa,  katika biashara nyingi ambazo mahitaji yake kwa wateja ni makubwa, huwezi kukuta zina  faida kubwa sana, lakini kwa kuwa mzunguko wake nao ni mkubwa basi faida ile ndogo ndogo huwa kubwa katika kipindi cha muda mfupi na ni ya uhakika kwani wateja ni lazima waje wanunue. Nasema ni ya uhakika kwani, hebu fikiria  kitu kama vocha ni sawa na chakula, mtu anapokula leo, kesho ni lazima njaa itamshika na atahitaji kula tena.

Hivyo ninachotaka kusisitiza hapa tu ni kwamba, ikiwa biashara ni endelevu, unaimudu kimtaji na soko lipo kwa maana ya wateja, usiangalie sana ukubwa wa faida bali zingatia zaidi mahitaji ya wateja wako huku ukitengeneza mkakati wa kupata wateja wengi zaidi, na kuhakikisha wale uliokuwa nao hawakukimbii, faida kidogokidogo hatimaye itakuwa kubwa na utashangaa  ikiwa ni biashara ileile uliyokuwa ukiidharau kuwa “hailipi, ni biashara kichaa”


Picha na Africa Business blog.




0 Response to "HAKUNA BIASHARA ISIYOKUWA NA FAIDA"

Post a Comment