HATARI! SODA ZA COLA HUYEYUSHA MISUMARI, MENO NA BETRI ZA MAGARI | JIFUNZE UJASIRIAMALI

HATARI! SODA ZA COLA HUYEYUSHA MISUMARI, MENO NA BETRI ZA MAGARI

Aina mbalimbali za soda.
Kwa muda mrefu sasa kumekuwa na mjadala mkubwa juu ya vinywaji baridi hususan soda na hasa zile zenye asili ya Cola, wengine wakidai ni hatari kwani vina uwezo wa kuyeyusha misumari, kusafishia terminal’ za betri za magari, uwezo wa kuyeyusha meno na hata ukioshea masinki ya choo basi yanatakata utafikiri umetumia jiki.

Lakini ni kitu gani kinachosababisha kinywaji hiki kuwa na sifa hizo? Kwenye soda hasa zile za Cola huwekwa kemikali, Asidi aina ya Citric, ambayo ndiyo chanzo cha kuwa na uwezo huo wa kumengenya vitu kiasi hicho. Lakini ikumbukwe kuwa acid hiyo haipatikani katika soda tu peke yake, kwani kumekuwa na watu wapotoshaji wanaotangaza ubaya wa soda kama kwamba ni kitu hatari zaidi kushinda vitu au vyakula vingine vilivyokuwa na kemikali hii ya citric acid.

Vyakula vingine ambavyo siyo soda lakini ndani yake vina asidi hii ni pamoja na matunda kama vile machungwa malimao, ubuyu, ndimu, ukwaju na hata soda zisizokuwa za cola. Kinachotofautisha soda za cola na zile zisizokuwa za cola ni kiwango tu cha citric acid iliyoko ndani yake, vya cola vina acidi nyingi zaidi.

Tunapozungumzia madhara yatokanayo na asidi ya soda za cola ni lazima tujiulize kwanza ikiwa citric acid yenyewe ni hatari kwa kiasi gani katika miili yetu, na ikiwa basi ni hatari je, vyakula vingine vyenye hii acid siyo hatari? Kwa hiyo na machungwa nayo tuyapige vita? Au citric ya matunda na ile ya kiwandani inayotiwa katika soda huwa zinatofauti fulani?

Kwa mujibu wa wataalamu wa kemia wanasema kwamba kemikali ya citric acid, imeunganishwa na atomi nyingi za Hydrojeni na hivyo kuifanya iwe rahisi mno kuyeyuka katika maji jambo linaloifanya isihifadhiwe mwilini kwa muda mrefu. Wanasema ili citric acid iweze kuwa sumu basi inabidi kiwango kikubwa sana cha kemikali hii kiingizwe mwilini kwa mara moja ndipo kiweze kuleta madhara.
CHUNGWA NA NDIMU.
Kimsingi wanasema kwamba citric acid ndiyo vitamin C yenyewe na inahitajika sana kwenye miili yetu katika kusaidia mfumo wa kinga za mwili “immune system” lakini inahitajika tu katika kiwango cha kadiri, nyingi zaidi inaweza ikaleta madhara.

Tukiachana na madhara yanayoweza yakasababishwa na citric acid kwa ujumla inapotumiwa katika kiwango kikubwa, yapo madhara mengine ambayo watu hawaelewi ni makubwa hata kushinda vile wanavyodhania kwamba husababisha ndani ya miili yetu.

Kuyeyusha meno! Acidi hii ina uwezo mkubwa wa kuyeyusha vitu vyenye asili ya chokaa kama meno na hata vitu vya asili ya chuma ndiyo maana watu wengi wamekuwa wakionyesha madhara yake kwa kusema “unapoweka msumari ndani ya chupa yenye cola siku kadhaa basi ukija kuuangalia huukuti tena”
 
SODA ZA KOPO
Sina uhakika na hilo lakini ni kweli kwamba citric acid inao uwezo wa ‘kula’ vitu vya chuma. Kuyeyusha msumari mzima mzima sijafanya utafiti kujua inachukua muda gani. Kuna wataalamu wengine wanaodai kwamba uwezo wa citric acid kusaga vitu ni karibu sawa na ule wa acid za maji ya betri na uwezo wa acid iliyoko ndani ya vinywaji vya cola ni mara 10 zaidi ya ule uliokuwa katika soda za kawaida. Lakini cha kustaajabisha zaidi ni kwamba ingawa soda za kawaida zina asidI kidogo kushinda zile za cola lakini zinasaga meno vizuri zaidi kushinda zile za cola.

Wakati acid za kwenye betri zina PH (kipimo cha asidi na alkali) namba 1.0, maji ya kawaida ambayo ni “neutral”,si acid wala alkali yana PH ya 7.0, soda za cola zina PH ya 2.5 wakati soda za kawaida ni 4.0. Katika utafiti uliofanyika mwaka 2006 ulibainisha pia kwamba acid kwenye machungwa nayo husababisha meno kumongonyoka lakini si kwa kiwango kikubwa kama ilivyokuwa kwenye soda. Kwa ujumla vinywaji vyote vinavyosindikwa viwandani huwekwa acid ambazo ni hatari kwa meno na ikiwa unajali meno yako na ungependa yabakie kuwa salama kwa muda mrefu basi ni kuvikwepa ama kutumia kwa kiwango kidogo sana.

JUISI HALISI YA MATUNDA
Richard Adamson Mwanasayansi mshauri kwenye taasisi inayojihusisha na vinywaji ya Marekani akiongea na jarida la “Live science” alisema hivi; “kinga kubwa uliyokuwa nayo mdomoni kwako ni mate ambayo hupoza acid, vipo vyakula vingi na siyo soda peke yake vinavyoweza kuozesha meno kama baadhi ya matunda, hakuna kigezo kimoja. Kinachotakiwa hapa tu ni kufurahia kila kitu kwa kadiri”.

 Anatoa ushauri kwa watu kutumia mirija “Straws” wakati wanapokunywa soda ili kupunguza ile hatari ya soda kugusana na meno na anasema njia ya kupunguza matumizi ya soda ni kwa kunywa soda wakati wa chakula.


CHANZO: Mitandao mbalimbali.

0 Response to "HATARI! SODA ZA COLA HUYEYUSHA MISUMARI, MENO NA BETRI ZA MAGARI"

Post a Comment