MABUTI YA NELSON MANDELA ALIYOSAHAU TANZANIA 1962 NA ASANTERABI NSILO SWAI MTU ALIYEYAHIFADHI AKAJA KUYARUDISHA 1995 | JIFUNZE UJASIRIAMALI

MABUTI YA NELSON MANDELA ALIYOSAHAU TANZANIA 1962 NA ASANTERABI NSILO SWAI MTU ALIYEYAHIFADHI AKAJA KUYARUDISHA 1995

Mabuti ya Nelson Mandela aliyosahau Tanzania miaka ya 60 yakaja kurudishwa na familia ya Bwana Nsilo Swai iliyoyahifadhi kwa miaka takriban 30.

Mabuti ya Nelson Mandela(Pichani Siyo yenyewe halisi bali huu ni mfano tu)  aliyosahau Tanzania leo hii yamekuwa gumzo kubwa katika hotuba ya Rais Jakaya Mrisho Kikwete aliposimulia jinsi familia ya Mtanzania mmoja aitwaye Asanterabi  Zefania Nsilo Swai aliyekuwa Mwekahazina wa Chamacha Tanu wakati huo na waziri wa viwanda na biashara ilivyohifadhi mabuti hayo kwa muda wa miaka 30 na kuja kuyarudisha kwa Madiba baada ya kuachiwa kutoka gerezani hapo mwaka 1995.

Kikwete alikuwa mmoja wa Viongozi wachache waliochaguliwa kutoa neno katika ibada hiyo ya mwisho kabla ya mazishi ya Tata Madiba Mandela, Shujaa wa Dunia. Wengine waliohutubia ni pamoja na Rais wa Malawi Bibi Banda ambaye naye hotuba yake ilishangiliwa sana na watu, Waziri mkuu wa Ethiopia, Rais wa zamani na rafiki wa Mandela Keneth Kaunda, Rais Jacob Zuma, Nandi Mandela mjukuu mkubwa wa Mandela na wengineo. Baada ya hotuba hizo watu wapatao 4,500 walikwenda kushuhudia Tata Mandela akipumzishwa katika nyumba yake ya milele kijiji cha Qunu mkoa wa Mashariki mwa Cape.

Kikwete alisimulia kwamba, Mandela hakupenda kukaa hotelini kutokana na sababu za kiusalama, na badala yake alikaa nyumbani kwa Bwana  Siro Swai mpaka alipoondoka kuelekea nchi zingine za afrika akaviacha viatu vyake(Mabuti ya kijeshi) aliyokuwa akiyatumia katika harakati zake za ukombozi kutoka serikali ya Makaburu ya Afrika Kusini kwa matumaini kuwa angerejea tena Tanganyika lakini kwa bahati mbaya alipofika nyumbani ndipo alipokamatwa na kufungwa miaka 27 jela. 

Katika ziara hiyo ya kwenda kumuaga kwa mara ya mwisho Rais Kikwete aliongozana na Mjane wake Nsilo Swai Bibi Vicky Nsilo Sway , mtu aliyemhifadhia Mzee Nelson Madiba Mandela buti zake kwa takribani miaka 30 bila kuchoka na hatimaye akaja kumrejeshea alipofunguliwa kutoka jela mwaka 1995, viatu vilimtosha sawasawa kama ilivyokuwa mwaka 1962.

Nelson Mandela alipokuja Tanzania mwaka 1962 katika harakati za kuanzisha mapambano ya msituni baada ya Makaburu kuonyesha hawakuwa tayari kabisa kukubali mapambano ya amani ya weusi kudai haki, alipokewa vizuri na Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliyeamini kwamba Tanzania isingeweza kuwa huru kikamilifu pasipo mataifa mengine ya Afrika kuwa huru hususanni yaliyokuwa kusini mwa Afrika; A. Kusini, Zimbabwe, Zambia , Angola na Msumbiji.

Madiba na wanaharakati wengine waliopewa hifadhi Tanzania ilibidi wapewe na vibali vya kusafiria na serikali ya Tanzania kusudi waweze kutembelea maeneo mbalimbali Afrika na Duniani kutafuta kuungwa mkono ambapo wasingeweza kupewa vibali hivyo na serikali ya madhalimu ya Makaburu wakati huo.

Ujasiri huo wa Mwalimu Nyerere ulikuwa wa kipekee kwani ilikuwa ni hatari mno kwa nchi iliyokuwa masikini sana kama Tanzania ukilinganisha na Makaburu waliokuwa tayari na uwezo mkubwa kijeshi na kiuchumi, Nyerere hakuogopa kutunguliwa na Makaburu akisafiri na ndege, kumbuka watu kama kina Samora Machel inasadikiwa huenda ndege yake ilitunguliwa na Makaburu hao hao.


0 Response to "MABUTI YA NELSON MANDELA ALIYOSAHAU TANZANIA 1962 NA ASANTERABI NSILO SWAI MTU ALIYEYAHIFADHI AKAJA KUYARUDISHA 1995"

Post a Comment